Dodoma FM

Wakala wa vipimo wafanya ukaguzi wa mizani Jijini Dodoma

20 May 2021, 2:31 pm

Na;MARIAM MATUNDU.

Ikiwa leo ni siku ya vipimo Duniani wakala wa vipimo Mkoani Dodoma  wametembelea na kufanya ukaguzi wa mizani katika maeneo ya hospitali na sehemu za kufanyia mazoezi.

Akizungumza katika ukaguzi huo kaimu meneja wa wakala wa  vipimo Mkoa wa Dodoma Karimu Zuberi amesema kutokana na kaulimbiu ya mwaka huu inayosema VIPIMO KATIKA AFYA ndio sababu iliyofanya kuadhimisha siku hii kwa kufanya ukaguzi katika mizani ya hospitali na sehemu za mazoezi.

Aidha amesema katika maeneo waliyopita wameridhishwa na hali ya mizani na kwamba kulikuwa na kasoro ndogo ndogo ambazo mafundi wamefanyia marekebisho.

Amesema ukaguzi wa mizani katika maeneo hayo ni muhimu kwakuwa inagusa afya za watu moja kwa moja na kuwataka wamiliki katika vituo vya kufanyia mazoezi na hospitali kuwa na utaratibu wa kuwaita wakala wa vipimo kufanya uhakiki wa mara kwa mara.

Kwa upande wao Rogers Malamsha katibu wa afya hospitali ya DCMC na Philipo ambaye ni mwalimu wa mazoezi wameshukuru wakala wa vipimo kutembelea maeneo yao na kufanya ukaguzi na kuahidi kuwa na utaratibu wa kuwaita wakala wa vipimo kwa ajili ya kufanya ukaguzi na kujiridhisha iwapo mizani wanayotumia ipo sawa.

Mei 20 kila mwaka huadhimishwa siku ya vipimo Duniani ambapo kwa mwaka huu maadhimisho hayo yamebebwa na kaulimbiu inayosema VIPIMO KATIKA AFYA, na  mkoa wa Dodoma kupitia wakala wa vipimo wamefanya ukaguzi katika hospitali ya DCMC na kituo cha kufanya mazoezi cha Home Fitness Center .