Dodoma FM

Mama lishe zingatieni usafi ili kuepusha maambukizi ya homa ya Ini

13 May 2021, 12:13 pm

NA; SHANI  NICOLOUS.

Wito umetolewa kwa mama lishe jijini Dodoma kuzingatia usafi katika shughuli zao, hususani wa vijiko vinavyotumika kulia chakula ili kuepusha maambukizi ya ugonjwa wa homa ya ini.

Akizungumza na Taswira ya Habari daktari kutoka Hospitali ya Benjamini Mkapa Dkt.Kessy Shija amesema kuwa ugonjwa huo ni rahisi kuenea kwa kuchangia kijiko kilichotumika na mgonjwa mwenye tatizo hilo.

Ameongeza kuwa mama lishe wanatakiwa kusafisha vijiko hivyo kwa maji ya moto yaliyochemka ili kuua vijidudu vinavyoweza kusambaza ugonjwa huo.

Aidha ameongeza kuwa ugonjwa huo pia unaenezwa kwa kuchangia vifaa vya kufanya usafi wa kinywa kama mswaki, kunyonyana ndimi na hata kushiriki ngono bila ya kutumia kinga, hivyo umakini unahitajika.

Kwa upande wao baadhi ya mama lishe jijini hapa wamesema kuwa wanatambua hatari ya ugonjwa huo hivyo mara nyingi hujitahidi kusafisha vijiko na vyombo vingine kwa maji moto.

Dodoma fm imezungumza na baadhi ya wananchi ambao wamesema ni vyema mamlaka zinazosimamia afya ziendelee kutoa elimu hii mara kwa mara.

Usafi katika maeneo ya kuuzia chakula pamoja na vyombo vinavyotumika ni muhimu kwani asilimia kubwa ya watu hujipatia milo yao katika maeneo mbalimbali yanayotolea huduma za vyakula ikiwemo kwa mama lishe.