Dodoma FM

Haki elimu yataja vipaumbele katika mabadiliko ya sera ya elimu

12 May 2021, 1:43 pm

Na; Mariam Matundu

Imeelezwa kuwa ili Tanzania kuwa na elimu jumuishi yenye ufanisi ni muhimu sera ya elimu ieleze wazi suala hilo na kuweka vipaumbele katika mitaala jumuishi ,pamoja na utoaji wa elimu nyumbufu kwa ngazi zote.

Hayo yameelezwa na mshauri mwelekezi kutoka haki elimu Wilberforce Meena na kuongeza kuwa mambo mengine ya kuzingatiwa katika kufanya mabadiliko ya sera ya elimu ni upimaji rekebishi wa wanafunzi,mpangobinafsi wa kujifunza kwa mwanafunzi pamoja na kuwaandaa walimu wenye uwezo.

Aidha amesema iwapo hayo yote yatakuwepo katika sera na yakatekelezwa kutakuwa na elimu jumuishi yenye ubora na ufanisi kwa makundi yote ya wanafunzi wenye ulemavu na kwamba wadau ni muhimu kushirikishwa katika mabadiliko hayo.

Nae mwalimu Joseph Degera kutoka shule ya Dodoma viziwi amesema elimu jumuishi bado inachangamoto nyingi kwa sasa ikiwemo suala la lugha kwa wanafunzi viziwi kujumishwa na wanafunzi wengine.

Kwa upande wake afisa elimu,elimu maalumu  msingi na sekondari Dodoma jiji Agnes Mwingira amesema bado kuna changamoto ya walimu wa elimu maalumu kupangiwa katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji tofauti ya alichokisomea.

Wadau mbalimbali wa elimu na watu wenye ulemavu wameendelea kutaka elimu jumuishi huku sera ya elimu 2014 na sheria ya elimu ya mwaka 1978 hazijatamka moja kwa moja elimu jumishi na badala yake suala hilo limetajwa katika sheria ya watu wenye ulemavu ya mwaka 2010 pamoja na sera ya taifa kuhusu huduma na maendeleo kwa watu wenye ulemavu ya mwaka 2004 pekee.