Dodoma FM

Uhaba wa Wafamasia, Serikali yaahidi kuajiri watumishi 10,467 maeneo mbalimbali.

7 May 2021, 1:52 pm

Na ; Yussuph Hans

Serikali imesema katika kutambua changamoto ya uhaba wa wafamasia nchini katika kipindi cha mwaka 2021/22 ina mpango wa kuajiri watumishi 10,467 ili kuhudumia maeneo mbalimbali nchini

Hayo yamesemwa Bungeni hii leo na Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mh.Festo Dugange wakati akijibu swali la mbunge wa Bukene Mh Selemani Jumanne aliyehoji Serikali ina mpago gani wa kuajiri wafamasia katika kila kituo cha afya ili kuimarisha usimamizi na mtiririko wa upatikanaji wa dawa.

Mh.Dugange amesema kwa mujibu wa ikama ya Watumishi wa afya, mtumishi wa famasia anapaswa kuwepo katika ngazi ya hospitali ambapo ngazi ya zahanati anapaswa kuwepo mteknolojia wa afya pamoja na msaidizi.

Akijibu swali la nyongeza la mbunge huyo, Mh Dugange amesema kuwa serikali ilitoa maelekezo kwa wakurugenzi wa halmashauri kutumia mapato ya ndani kuwaajiri wataalamu hao katika maeneo yenye uhaba wa wataalamu, ili kutatua changamoto hiyo katika vituo vya Afya.

Katika hatua nyingine Spika wa Bunge Mh.Job Ndugai amesisitiza juu ya vyama vyenye kuhitaji kuwafukuza wabunge wao ni vyema kufuata taratibu zilizopo ikiwemo kuandika barua itakayopita kwa msajili wa vyama vya siasa na kuambatanisha katiba na muhtasari wa vikao vilivyofanyika vya kuwafukuza wanachama husika.

Bunge limeendelea leo Jijini Dodoma ambapo wabunge pia wameendelea kuchangia hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Maji kwa mwaka 2021/22.