Dodoma FM

Wananchi watakiwa kutunza utamaduni kujenga Taifa lenye utambulisho stahiki

5 May 2021, 11:37 am

Na; Fred Cheti

Katika kuelekea siku ya uwanuai wa tamaduni duniani wito umetolewa kwa jamii kutunza na kuendeleza tamaduni za kitanzania katika ngazi zote ikiwemo  vitu vya asili ili kujenga Taifa lenye utambulisho stahiki na amani.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi Wizara ya habari, Utamaduni, Sanaa na michezo idara ya maendeleo ya Utamaduni Dkt.Emanuel Temu wakati akizungumza na Taswira ya habari ambapo amesema kuwa ni lazima jamii ihakikishe inaondokana na mambo mengi ya utandawazi  ambayo yatasababisha tamaduni za kitanzania kupotea.

Akizungumzia maadhimisho hayo ambayo yanatarajia kufanyika  Mei 21 mwaka huu Dkt.Temu amesema kuwa wizara imeaandaa kongamano la  urithi wa ukombozi lenye lengo la kujadili kwa kina mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Bara la Afrika.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kutoka wizara hiyo Bw.John Maperele amesema kuwa wizara imeweka mikakati kambambe ya kusimamia sekta hizo nne zilizo chini ya wizara yao ili kuhakikisha zinakua na tija kubwa kwa Taifa kiuchumi na kimaendelo.

Utamaduni ni mfumo wa maisha ya watu jinsi wanavyoishi na maendeleo yao kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiuchumi ambapo nchi ya Tanzania ni moja kati ya nchi zinazosifika Duniani kwa kulinda maadili yao ambapo kuna makabila yasiyopungua 120 ambayo hutunza mila na desturi zao.