Dodoma FM

Wakazi Iyumbu wataka ufafanuzi wa asilimia 45 makato ya viwanja

30 April 2021, 8:57 am

Na; Mariam Kasawa.

Wakazi wa mtaa wa Iyumbu Jijini Dodoma  wameutaka uongozi wa mtaa huo kutoa ufafanuzi wa makato ya asilimia 45 wanazokatwa na jiji kwa kila kiwanja wanachopewa baada ya upimaji wa hivi karibuni bila kujali kipo kwenye makazi au eneo la wazi.

Sambamba na hilo wametaka kujua idadi ya viwanja vilivyopatikana kutokana na makato ya asilimia hizo na kwamba kazi gani vitafanya baada ya kukamilika kwa zoezi hilo kwani katika barua hizo kumekuwa na kipengele cha malipo ya garama za upimaji ambazo kila mwananchi ametakiwa kulipa

Wananchi hao waliomba ufafanuzi huo kwenye mkutano wa hadhala uliofanyika mtaani hapo huku ukiwa na ajenda kadhaa zikiwemo za kuitambulisha kampuni ya uchimbaji madini ambayo itakuwa ikichimba kifusi kwenye moja ya milima iliyozunguka mtaa huo, Ulinzi na usalama na taarifa ya upimaji na ugawaji viwanja  na changamoto zake.

Akizungumza  kwenye mkutano huo Nason Lugunyale mkazi wa mtaa huo amesema ugawaji huo unaoendelea haujazingatia makubaliano ya mikutano ya awali ambayo walikubaliana kabla ya kuanza kwa upimaji na ambayo yapo kwenye andiko la mkataba.

Amesema kwenye makubaliano hayo walikubaliana na jiji kuwa kutakuwa na makato ya asilimia 30 kwenye eneo la wazi lakini kwenye makazi hakutakuwa na makato yoyote

Kwa upande wake Mwenyekiti wa kamati ya upimaji  bw.Noel Chipanga ametaja jumla ya viwanja 1472 vilipatikana katika upimaji 1210 vimeshagawiwa kwa wahusika na kwamba kumekuwa na changamoto ndogondogo ambazo aliwataka wahusika kuziandika kwenye daftari la mtendaji wa mtaa ili zije kutatuliwa na maafisa ardhi wa jiji hilo.

Chipanga amesema pamoja na ugawaji huo unaoendelea hata yeye kama mwenyekiti wa kamati hajui idadi kamili ya viwanja vilivyopatikana kutokana na  asilimia walizokatwa wananchi, vitafanya kazi gani wakati ni kweli wananchi wanalipia gharama za upimaji na kwamba atafuatilia na kuja kuitolea majibu.