Dodoma FM

TACAIDS yawajengea uwezo wasichana kutambua haki zao

30 April 2021, 12:01 pm

Na; Mariam Matundu.

Tume ya kudhibiti  Ukimwi nchini TACAIDS  chini ya  uratibu wa masuala ya ukimwi kwa mtazamo wa kijinsia imetoa mafunzo kwa wasichana na wanawake wanaoishi na virusi vya ukimwi ili kuwapatia utambuzi wa haki zao za msingi katika maeneo yao.

Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo afisa jinsia kutoka Tacaids Bi.Judith Luande   amesema lengo la  uwezeshaji huo ni kuwapa elimu ili waweze kuzifikia huduma msingi hususani kwa kundi la walemavu wanaoishi na virusi vya ukimwi.

Amesema katika makundi maalum hususani walemavu wanakutana na vikwazo katika kupata huduma zao  za msingi kutokana na baadhi yao kutokuwa na vipato vya uhakika vinavyowawezesha kufika katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya kupata huduma hizo.

Kwa upande wao washiriki wa mafunzo hayo wamesema wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo magonjwa nyemelezi na unyanyapaa kutokana na kuishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi.

Tume ya kudhibiti  ukimwi nchini tacaids  chini ya  uratibu wa masuala ya ukimwi kwa mtazamo wa kijinsia wakishirikiana na wadau wengine  wametoa mafunzo kwa wasichana na wanawake wanaoishi na maambukizi ya virusi vya ukimwi yaliyofanyika jijini Dodoma.