Dodoma FM

RAIS SAMIA SULUHU ASHINDA KWA KISHINDO UENYEKITI CCM

30 April 2021, 1:22 pm

Na; Alfred Bulaya.

Mkutano mkuu maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao umefanyika jijini Dodoma hii leo, umemchagua Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa Mwenyekiti mpya wa CCM Taifa.

Rais Samia Suluhu Hassan ameteuliwa na wajumba baada ya kupigiwa kura zote 1, 862 zilizopigwa na Wajumbe wa mkutano mkuu maalum wa CCM, na kuwa Mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Mwenyekiti wa CCM Taifa.

Akizungumza baada ya kuchagulia Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kazi ya kukiimarisha Chama Cha  Mapinduzi inaendelea huku akibainisha kuwa hatawaangusha wanawake na watanzania kwa ujumla.

Ameongeza kuwa chama hicho kinakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo baadhi ya viongozi wake kukosa vitendea kazi hivyo ni wakati sasa wa kufanyia kazi jambo hilo.

Pamoja na hayo amesema siasa si uadui hivyo kuviomba vyama vya siasa kutoa ushirikiano katika kuimarisha umoja uliopo kwani Ushindi wa CCM  mwaka 2025 utaletwa kwa namna wana CCM watakavyotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho.

Aidha mkutano huo umeridhia mapendekezo ya yaliyotolea na mwenyekiti wa CCM kujaza nafasi kadhaa na kufanya mabadiliko katika sekretarieti kuu ya chama hicho. Katika mabadiliko hayo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw.Daniel Chongolo ameteuliwa kuwa katibu mkuu wa CCM akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Dkt.Bashiru Ally huku katibu wa itikadi na uenezi akipitishwa Bw.Shaka Hamdu Shaka kuchukua nafasi ya Ndg.Hamfrey Polepole.