Dodoma FM

Mpalanga wakabiliwa na changamoto ya wahudumu wa Afya

27 April 2021, 11:39 am

Na; Victor Chigwada

Kituo cha afya kilichopo katika Kijiji cha Mpalanga Wilayani Bahi kinakabiliwa na upungufu wa wahudumu wa afya pamoja na mganga mkuu hali inayodhohofisha utoaji huduma.

Hayo yamebainishwa na baadhi ya wananchi wa Kata hiyo wakati wakizungumza na taswira ya habari ambapo wameiomba Serikali iwaongezee wahudumu wa afya pamoja na mganga mkuu ili kuwatatulia changamoto hiyo.

Mwenyekiti wa Kijiji hicho Bw.Mnyukwa Sakaila amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo huku akiongeza kuwa wanakabiliwa na  upungufu wa majengo ikiwa ni pamoja na vyumba vya mapumziko.

Diwani wa Kata ya Mpalanga Bw.Baraka Ndahani amesema kuwa walishapeleka maombi ya kupatiwa mganga mkuu katika kituo hicho  lakini hawajapewa majibu.

Sekta ya afya Wilaya ya Bahi bado ina upungufu  mkubwa wa watumishi kwani hadi sasa kuna jumla ya watumishi 369 kati ya 779 wanaohitajika na hivyo kuwa na upungufu wa watumishi 410.