Dodoma FM

Akina mama wajawazito washauriwa kutumia unga ulioongezwa virutubishi

27 April 2021, 8:53 am

Na;Jayunga Pius

Wanawake walio katika umri wa kujifungua wameshauriwa kutumia chakula aina ya ugali unatokana na unga ambao umeongezwa virutubishi ili kuepuka kujifungua watoto walio na matatizo mbalimbali ya kiafya ikiwemo kichwa kikubwa na mgongo wazi.

Ushauri huo umetolewa na meneja mwandamizi wa shirika la Project Health Tanzania (SANKU) Bw. Gwao Omary Gwao wakati akizungumza na kituo hiki juu ya hali ya utapiamlo Nchini na hasa kundi la watoto.

Amesema jamii imekuwa ikiona fahari kutumia chakula cha ugali ambao unatokana na mahindi yaliyo kobolewa na kuondolewa vitamin muhimu ikiwemo madini ya chuma na hivyo kusababisha mama kujifungua mtoto alie na mapungufu kiafya ikiwemo upungufu wa damu mwilini, uwezo mdogo wa kufikiri na kutunza kumbukumbu.

Bw. Gwao ameishauri jamii kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya na lishe Nchini ili kuepuka changamoto za kudhoofu kiafya ikiwemo tatizo la utapiamlo na hasa kundi la watoto na kwamba jamii ijenge utamaduni wa kununua vyakula vyenye virutubishi maalumu kwa kuzingatia nembo ya Serikali katika bidhaa hizo ikiwemo mafuta ya kula, unga wa ngano na unga wa mahindi.

Hivi karibuni Dodoma Fm ilizungumza na Afisa lishe wa Jiji la Dodoma Bi. Penieva Juma na kueleza kuwa swala la utapiamlo lisipochukuliwa hatua za haraka katika kulitokomeza husababisha utapiamlo ambao ni sugu na waathirika wakubwa katika hilo wakiwa ni watoto wadogo chini ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2015/2016 Nchini zinaonesha 35% ya watoto wa kitanzania ni wadumavu wa kimo ikilinganishwa na umri wao, 58% ya watoto walikuwa na upungufu wa damu na 45% ya wanawake walio katika umri wa kuzaa walikuwa na upungufu wa damu.