Dodoma FM

Wakazi Chilonwa waomba uongozi wa Chamwino kuhamisha Dampo ambalo limekuwa kero kwao

16 April 2021, 12:02 pm

Na; Selemani kodima

Dampo la kutupia taka lililopo katikati ya mpaka wa Kijiji cha Chamwino ikulu  na Chilonwa Wilayani Chamwino limetajwa kuhatarisha afya za wananchi wa eneo hilo..

Hayo yamefahamika baada ya Taswira ya habari kuzungumza na baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Chilonwa ambao wamekuwa ni waathirika  wakuu wa maji machafu yanayotiririka kutoka katika dampo hilo ambalo limekuwa likitumiwa na Serikali ya Kijiji cha Chamwino ikulu.

Adam Ndoma ni mkazi wa Chilonwa amesema  uwepo wa dampo hilo ni hatari kwa usalama wa afya zao kutokana na maji yaliyobeba taka kutiririka wakati wa mvua hadi kwenye makazi yao.

Nae mtendaji wa Kata ya Chilonwa Bw .Khatibu Nassoro amesema hatua walizochukua ili kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo ni kufanya mawasiliano na uongozi wa Kijiji cha Chamwino ambapo umeomba kupewa muda ili kutatua tatizo hilo .

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Chamwino   Bw.Peter Kalaita  ametolea ufafanuzi juu ya kero hiyo ambapo amekiri kuwa walinunua eneo hilo baada ya dampo la kwanza kujaa hivyo wanatarajia kuchimba dampo mwishoni  mwa mwezi huu ili kuondoa kero kwa wananchi.

Pamoja na hayo Diwani wa Kata ya Chamwino Bw. Joseph Maguo amesema ili kufanikisha zoezi hilo atasimamia kwa karibu kwa kushirikiana na  afisa afya ili kuhakikisha wanalinda usalama wa wananchi wa pande zote.