Dodoma FM

Waislamu watakiwa kutumia kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhani kujinyenyekeza kwa Mungu

14 April 2021, 11:32 am

Na;Yussuph Hans                 

Wakati hii leo waumini wa dini ya Kiislamu wakianza mwezi mtukufu wa Ramadhan, wito umetolewa kwa waumini hao kujizuia kufanya mambo yote yaliyokatazwa na Mwenyezi Mungu ili kutimia kwa lengo la funga zao.

Akizungumza na taswira ya Habari Sheikh Abdul Shakuru kutoka Msikiti wa Maili Mbili jijini Dodoma, amesema ni vyema Waislamu wakijiepusha na mambo yote yanayoharibu saumu zao kama mafundisho ya kiislamu yanavyoelekeza.

Aidha Sheikh Shakuru amesema kuwa ni vyema Waislamu kutumia kipindi cha Mfungo wa Ramadhani kujinyenyekeza kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kufanya  ibada mbalimbali kwa wingi.

Moja ya changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza katika msimu wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali, ambapo  taswira ya habari imezungumza na baadhi ya Wafanyabiasha na Wananchi jijini hapa ambapo wamesema bei za baadhi ya bidhaa zimepanda kwa wastani.

Waumini wa Dini ya Kiislamu Nchini wanaungana na waumini wengine  Duniani kote kufunga Ibada ya mwezi mtukufu wa ramadhani ikiwa ni nguzo ya Nne katika Uislamu.