Dodoma FM

TBS Yateketeza Bidhaa Zenye Thamani ya Milioni 19

14 April 2021, 8:05 am

Na ; Mariam Kasawa.

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeteketeza bidhaa hafifu za vyakula na vipodozi zenye thamani ya shilingi milioni 19 katika maeneo mbalimbali ya biashara katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa Mujibu  wa Meneja wa Shirika hilo Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Abel Mwakasonda,  bidhaa hizo hafifu zilikamatwa wakati wa ukaguzi wa bidhaa sokoni uliofanyika katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2021 katika mikoa ya Iringa, Njombe, Songwe na Mbeya.

Bidhaa hizo ni pamoja na vinywaji aina ya soda,bia, vyakula kama biskuti,mafuta ya kula, siagi na sabuni za kuogea ambazo muda wake wa matumizi umekwisha.

Vilevile vipodozi vilivyokamatwa ni vile visivyoruhusiwa kuingizwa hapa Nchini kutokana na kuwa na viambata sumu kama vile madini tembo (lead), zebaki (Mercury) na Hydroquinone.

Matumizi ya vipodozi hivyo vyenye viambata sumu yana madhara kiafya ambayo husababisha magonjwa ya saratani kwa binadamu, na kwamba, vyakula vilivyokwisha muda wa matumizi husababisha magonjwa ya homa za matumbo.

Aidha, Taarifa hiyo inaeleza kuwa matumizi  ya bidhaa hafifu huleta madhara ya kiuchumi kwa muuzaji na mnunuzi wa bidhaa husika baada ya kuthibitishwa kuwa bidhaa hizo hazifai kwa matumizi ya binadamu na kutakiwa kuondolewa sokoni na kuharibiwa.

Ukaguzi wa bidhaa sokoni unafanywa kwa kuzingatia sheria ya Viwango Na 2 ya mwaka 2009 na  Sheria ya Fedha Na 8 ya mwaka 2019 ambayo ilihamisha majukumu ya usajili wa majengo ya vyakula na vipodozi yaliyokuwa yakifanywa na iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) kwenda kwa TBS.

Shirika linatoa rai kwa wauzaji wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha kuwa wanaingiza sokoni bidhaa ambazo TBS imethibitisha ubora wake na kuziondoa sokoni bidhaa zilizokwisha muda wake wa  matumizi badala ya kuendelea kuziuza.