Dodoma FM

Mzee Mwinyi amtembelea Rais Samia Nyumbani kwake

12 April 2021, 1:44 pm

Na; Mariam Kasawa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo tarehe 12 Aprili, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili,  Dkt. Ali Hassan Mwinyi ambaye amempongeza kwa kuanza vizuri majukumu yake ya kuongoza Nchi.

Akizungumza baada ya mazungumzo yao, Dkt. Mwinyi amesema amefika nyumbani kwa Mhe. Rais Samia kumjulia hali, kumtia moyo na kumhakikishia kuwa yeye na Wazee wenzake wapo tayari kutoa ushirikiano na kumsaidia wakati wowote watakapohitajika kufanya hivyo.

Akizungumza  Dkt. Mwinyi amesema “Mama ameanza vizuri, ingekuwa ni nyimbo ningesema once more!!!, ameanza vizuri kabisa na kila mmoja ana furaha, kila raia unayemsikia anasema Mama ameanza vizuri, tuliyekuwa nae tulikuwa na Rais mzuri sana, mzoefu wa mambo ya kiserikali, ametufanyia kazi nzuri sana, sasa kaacha mambo haya ghafla kamuachia mwenzie, sasa Mama naye mwanadamu atakuwa na yake na vile vile kuna mambo ambayo yameanzwa na mtu mwingine  ambayo watu wanayataka wanayapenda, wanamshikilia Mama tunayataka haya tunayataka!!, tulieni tutayatekeleza haya, sasa hilo linafurahisha”.

Rais Mstaafu Mwinyi amewataka Watanzania kumuunga mkono Mhe. Rais Samia kwa kuacha balaa, ugomvi na fitina badala yake wawe na umoja, mshikamano na kufanya juhudi za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.