Dodoma FM

Serikali yajipanga kutatua changamoto inayo vikabili vituo vya Afya mwaka wa fedha 2021/2022

6 April 2021, 1:54 pm

Na Suleiman Kodima

Naibu waziri ofisi ya Rais Tamisemi  Dkt Festo Dugange amesema Serikali inatambua  uhitaji wa wahudumu wa afya , Vifaa tiba na Gari la kubebea wagonjwa katika Hospitali ya Uhuru hivyo wanategemea suala hilo Kuwa sehemu ya Utekelezaji mwaka fedha 2021/2022.

Hayo ameyasemwa Bungeni leo katika kipindi cha Maswali na majibu ,wakati akijibu  swali la Nyongeza la Mbunge wa Viti maalumu Fatma Tawfiq ambaye ametaka kujua Serikali inatoa maelezo gani juu ya upungufu wa wafanyakazi katika hospitali ya uhuru iliyopo wilayani Chamwino pamoja na kukosekana kwa Gari la kubebea wagonjwa.

Akijibu swali hilo ,Naibu Waziri Dkt Dugange amesema serikali inatambua umuhimu wa hospitali ya Chamwino  katika kuboresha huduma za afya kwa jamii na suala la watumishi wa kutosha ,vifaa tiba na Gari la wagonjwa

Amesema jambo hilo lipo katika mipango ya utekelezaji wa mwaka wa fedha ujao 2021/2022 na serikali itahakikisha watumishi watakao ajiriwa wanapelekwa katika hospitali ya uhuru na kufanya utaratibu wa kupata Gari la wagonjwa na vifaa tiba ili hospitali hiyo ianze kutoa huduma kwa wananchi.

Pamoja na hayo amesema serikali inatambua uhitaji wa idadi ya watumishi wa afya katika maeneo mbalimbali ambapo mpango wa serikali  katika vituo vya afya kwa mwaka wa fedha ujao wanatarajia kuomba Shilingi Bilioni 22.5 kwa ajili ya kuhakikisha vituo vyote na hospitali za halmashauri zilizojengwa zinapata vifaa tiba kwa kushirikiana na mapato ya ndani ya Halmashauri.