Dodoma FM

Philip Mpango athibitishwa kuwa Makamu wa Rais Tanzania

30 March 2021, 8:54 am

Na; Mariam Kasawa

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, kupitia kwa mpambe wake, leo Machi 30, amewasilisha Bungeni jina la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. .

Jina hilo liliwasilishwa bungeni asubuhi ya leo Jumanne machi 30 na mpambe wa rais katika bahasha maalum.Baada ya kupokea Spika Job Ndugai alilitangazia bunge jina hilo lililopendekezwa na Rais Samia.

Mara baada ya tangazo hilo bunge lililipuka kwa shangwe.

Bwana Mpango amekuwa waziri mwandamizi katika serikali ya hayati John Magufuli akihudumu kama waziri wa fedha

Kuanzia miaka ya 1990 hadi 2000, alifanya kazi akiwa mhadhiri mwandamizi wa uchumi katika kitivo cha Biashara (sasa Shule ya Biashara) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Alikuwa akifundisha “Microeconomics”, “Macroeconomics” (kwa mwaka wa pili) na “Public Finance” kwa mwaka wa tatu na kozi za uzamili. (Kwa tafsiri yangu, Uchumi mdogo, Uchumi mkubwa na masuala ya Fedha za umma.)

Amewahi kuwa Mchumi Mwandamizi wa Benki ya Dunia, Mkuu wa Kamati ya kumshauri Rais Jakaya Kikwete wakati huo kuhusu masuala ya uchumi, Katibu binafsi wa Rais anayeshughulikia masuala ya uchumi, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, kabla ya kuhamishiwa Tume ya Mipango, Ofisi ya Rais.

Nyadhifa hizi zote amezishika wakati wa utawala wa Kikwete.

Hayati Magufuli alipoingia madarakani alimteua kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na baada ya siku chache akateuliwa kuwa Waziri wa Fedha na Mipango.

Katika uchaguzi wa mwaka 2020 alishinda kiti Cha ubunge jimbo la Buhingwe.

Kisha kuteuliwa tena kuwa waziri wa fedha na Mipango.