Dodoma FM

C Sema na TADIO zawajengea uelewa waandishi juu ya ukeketaji na ndoa za utotoni

13 March 2021, 9:35 pm

Na,Rabiamen Shoo. Arusha.

Asasi isiyo ya kiserikali ya C Sema na mtandao wa radio za kijamii Tanzania TADIO, wakiwezeshwa na UNFPA zimefanya kikao kazi cha siku mbili na waandishi wa habari kutoka redio za kijamii, kuwajengea uwezo wa namna ya kutoa elimu na kuripoti vitendo vya ukeketaji kwa wanawake na ndoa za utotoni.

Akizungumza katika mafunzo hayo mdau wa mawasiliano na mahusiano ya jamii Bi.Irene Makene amesema redio za jamii ndizo zenye nafasi kubwa ya kutoa elimu kwa jamii zaidi kwa kuwa zipo karibu nayo kwa kushirikiana na wadau wengine.

Lengo la kikao kazi hiki cha siku mbili ni kujadiliana, na kuweka mikakati ya jinsi gani ya kuweka nguvu ya pamoja katika mapambano ya kupinga ukatili wa kijinsia na ndoa za utotoni” amesema Bi.Irene Makene.

Bi.Irene Makene ambaye ni mdau wa mawasiliano na mahusiano ya jamii

Bw.Franciss Selasini kutoka taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na mapambano dhidi ya ukeketaji na ndoa za utotoni NAFGEM, amewataka wanahabari kuwa mstari wa mbele katika mapambano haya kwa kutoa elimu kwa jamii, kufichua na kuripoti matukio hayo ili wahusika wachukuliwe hatua na kutoa msaada kwa waathirika wa vitendo hivyo au hata waliopo katika hatari ya kufanyiwa ukatili huo.

Bw.Franciss Selasini (aliyesimama) kutoka NAFGEM akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari

Naye Bw.Michael Marwa ambaye ni mkurugenzi kutoka shirika la C Sema linalojihusisha na malezi na makuzi ya mtoto, amesema wamekuwa wakishirikiana na wadau wakiwemo wanahabari katika kuhakikisha kuwa mtoto anaishi maisha salama huku wakifanyia kazi haraka wanapopata taarifa za ukatili kwa mtoto popote nchini.

Bw.Michael Marwa kutoka C Sema akitoa mafunzo kwenye kikao kazi hicho

Awali akifungua mafunzo hayo, afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya jiji la Arusha Bi.Angella Kiama, amewataka waandishi wa habari kutumia weledi walioupata kuongeza nguvu katika kupinga ukatili kwa wanawake na watoto kwa kuwa wana nafasi kubwa ya kufanya hivyo kwenye jamii, na sio kuwaachia wadau pekee.

Kikao kazi hicho ambacho Dodoma Fm nayo imeshiriki, Mikoa sita imetajwa kuongoza katika matukio ya ukatili hususan  ukeketaji ambapo Manyara inaongoza ikifuatiwa na Dodoma, Arusha, Singida, Mara na Tanga.