Dodoma FM

Zaidi ya trilion 1 zawekezwa sekta ya elimu nchini

9 March 2021, 8:32 am

Na, Yussuph Hans,

Dodoma.

Imeelezwa kuwa zaidi ya shilingi trilioni 1.291 zimewekezwa katika mpango wa elimu bure, ambapo matokeo yake yameonekana kwa kuongezeka kwa idadi kubwa ya wanafunzi Shuleni pamoja na Ufaulu.

Hayo yamebainishwa na msemaji mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu Wizara ya Habari Dkt.Hassan Abbas hapo jana wakati akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dodoma, juu ya Sekta ya maji pamoja na elimu zilivyopiga hatua katika kipindi cha Utawala wa Rais Dkt.John Pombe Magufuli.

Dkt.Abbasi amesema kuwa kuna maboresho makubwa yaliofanywa katika Sekta ya elimu nchini ikiwemo miundombinu ya Shule, Vifaa vya Elimu pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu.

Pamoja na hayo amesema Serikali imeongeza kiwango cha mikopo kwa taasisi za elimu ya juu kwa kuongeza kiwango cha mikopo hali ambayo pia imesaidia ongezeko la idadi ya wanafaunzi Vyuoni.

Abbasi amesema kuwa huduma ya maji imeboreshwa ambapo kutokana hatua mbalimbali zilizofanyika ikiwemo kuanzishwa kwa wakala wa maji Usafi na Mazingira Ruwasa, na kuongezeka kwa huduma ya maji taka na Safi.

Aidha amesema hali ya upatikanaji wa maji nchini kwa sasa katika awamu ya tano ya Rais Dkt.John Pombe Magufuli imeongezeka, ikiwemo kutoka Asilimia 47-74% Vijijini ambapo kulikuwa kuna adha hiyo kwa kiasi kikubwa.