Dodoma FM

Dodoma Jiji Fc wasaka rekodi

9 March 2021, 9:14 am

Na, Rabiamen Shoo,Dodoma.

Kikosi cha Dodoma Jiji kikiwa mazoezini

Timu ya Dodoma Jiji Fc hii leo inatarajia kushuka katika dimba la Sokoine jijini Mbeya kuvaana na wenyeji wao Mbeya City Fc kwenye mechi ya ligi kuu soka Tanzania Bara.

Dodoma jiji hivi karibuni imeibuka na ushindi katika mechi mbili mfululizo,ambapo ilianza kuitandika 7- 0 Kipigwe Fc kwenye mechi ya kombe la Shirikisho ASFC, ambapo pia walisafiri hadi Mkoani Pwani kuvaana na Ruvu Shooting kwenye mechi ya ligi na kuwafunga maafande hao bao 2-0 katika dimba la Mabatini.

Pamoja na mafanikio hayo ya ushindi mfululizo, mshambuliaji wa klabu hiyo Anwar Jabir amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Februari kutokana na kuisaidia timu yake kushinda katika mechi hizo.

Kwa mujibu wa afisa habari wa klabu hiyo Mosses Mpunga, hii leo walima zabibu hao watashuka dimbani kwa nia moja ya kuibuka na ushindi ili kuendeleza pale walipoishia, huku wakitambua kuwa Mbeya City ni timu ngumu na yenye uzoefu katika ligi kuu.

Dhamira yetu sisi Dodoma Jiji ni kubakia katika nafasi tano za juu,kwakuwa sisi tunastahili kuwa katika nafasi hizo, lakini kilichofanya tushuke nafasi mbili ni kutokana na kuwa nyuma mchezo mmoja,na leo tutarejea nafasi yetu” amesema Mosses.

Dodoma Jiji wapo nafasi ya saba wakiwa na pointi 32 huku wakicheza mechi 22 mechi moja pungufu ya timu zilizopo juu yake KMC Fc na Ruvu Shooting, na endeapo watashinda leo watapanda hadi nafasi ya tano kwenye msimamo.

Mbeya City yenyewe ipo nafasi ya 17 ambayo ni nafasi ya pili kutoka mkiani wakiwa na pointi 16 baada ya kucheza michezo 21 huku timu inayoburuza mkia ikiwa ni Mwadui Fc yenye pointi 16 pia.