Dodoma FM

Mpango mwingine wa miaka 10 waanzishwa kupunguza ajali

9 February 2021, 2:11 pm

Na,Mariam Matundu,

Dodoma.

Kufuatia mpango kazi wa Dunia wa kuzuia ajali za barabarani kwa asilimia 50% wa miaka kumi iliyopita 2011 hadi 2020 kutokufika malengo, umeanzishwa mpango mwingine wa miaka 10, 2021 hadi 2030 unaoendana na malengo ya maendeleo endelevu.

Kupitia mpango kazi huu nchi zimetakiwa kujipima kupitia viashiria vya kupunguza ajali pamoja na kuwa na mipango ya muda mfupi na muda mrefu ya mikakati ya kupunguza ajali inayohusisha wadau mbalimbali.

Akizungumza na kituo hiki mratibu wa mradi wa usalama barabarani nchini Tanzania chini ya Shirika la afya Duniani Mery Kesi, amevitaja viashiria vinavyoweza kusaidia nchi kufikia malengo kuwa ni pamoja na mabadiliko ya sheria ya usalama barabarani.

Akiwakilisha wadau wa usalama barabarani, mbunge wa viti maalumu Mkoa wa Shinyanga Salome Makamba, amesema licha ya sheria ya usalama barabarani kupitwa na wakati pia kuna mapungufu ya utoaji wa elimu kwa makundi mbalimbali.

Takwimu za usalama barabarani za mwaka 2020 zinaonesha kupungua kwa ajali ambapo ziliripotiwa ajali 1602, vifo 1157 na majeraha 1985, ikilinganishwa na mwaka 2019 ajali zilikuwa 2525, vifo 1351 na majeraha 2621 huku makosa ya kibinadamu yakitajwa kusababisha ajali kwa asilimia 78%, ubovu wa vyombo vya moto 16% na vyanzo vingine ikiwemo ubovu wa barabara 8%.