Dodoma FM

Waziri Mkuu:Wekeni mipango ya kudumu ujenzi wa miundombinu ya shule

4 February 2021, 12:59 pm

Na,Mariam Matundu,

Dodoma.

Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini kuwa na mpango wa kudumu unaosimamia ujenzi wa miundombinu katika shule zote, ili kuepuka upungufu wa madarasa unaokwamisha baadhi ya wanafunzi kushindwa kuanza kidato cha kwanza .

Akizungumza Bungeni hii leo katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo, Waziri mkuu Mh.Kassim Majaliwa amesema ni wakati sasa Halmashauri kutumia takwimu za wanafunzi waliopo ili kujenga miundombinu ya kutosha kila mwaka, na kuacha kufanya zoezi hilo kuwa la kushtukiza.

Moja ya madarasa yaliyopo kwenye ujenzi

Wakati huo huo mbunge wa viti maalumu kupitia CHADEMA Kunti Majala, ameiuliza Wizara ya Tamisemi ni lini Serikali itapeleka walimu wa kike katika shule za msingi Bilise na Dosee zilizopo wilaya chemba kwa kuwa wilaya hiyo inaupungufu wa walimu wa kike kwa kiwango kikubwa .

Akijibu swali hilo naibu Waziri wa TAMISEMI Mh.David Silinde amesema tayari Serikali imepeleka mwalimu mmoja wa kike katika shule ya Bilise na kwamba katika mpango wa kuajiri walimu Wizara itazingatia jinsia kwa maslahi ya wanafunzi wa kike kote nchini.

Moja ya madarasa yaliyopo katika hatua za mwisho kukamilika

Leo kikao cha tatu katika Bunge la 12 kimeendelea jijini Dodoma, ambapo kimetanguliwa na maswali ya papo kwa papo kwa waziri mkuu, na baadae kipindi cha maswali na majibu kwa Wizara mbalimbali.