Dodoma FM

Prof.Mkenda:Tunatilia mkazo uzalishaji mazao ya mafuta

25 January 2021, 8:59 am

Prof.Adolf Mkenda

Na,Alfred Bulaya,

Dodoma.

Serikali imesema inaweka nguvu kubwa katika uzalishaji wa mazao ya mafuta ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mafuta inayotokea nchini na kupunguza kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi.

Mkazo huo unawekwa kwa kuzingatia kwamba ni asilimia 47 tu ya mahitaji ya mafuta ndio yanazalishwa nchini na kama nchi inatumia karibu nusu trilioni kuagiza mafuta kutoka nje.

Akizungumza mara baada ya kutembelea kiwanda cha mafuta ya alizeti cha PYXUS kilichopo Kizota jijini Dodoma,Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda amesema ni wakati sasa wa wakulima kuandaa mashamba na kutumia mbegu bora na watalaam.

Profesa Mkenda amekemea suala la urasimu lililopo bandarini katika utoaji wa vibali vya usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi na kusema yeyote mwenye tabia hiyo atafute shughuli nyingine ya kufanya.

Naye meneja wa wakulima wadogo wa Pyxus Edwin Shio, ametaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na wakulima kukiuka masharti yaliyopo kwenye mkataba, na kupata kibali cha kusafirisha mafuta ghafi kwenda nje ya nchi.