Chai FM

Siku ya kimataifa ya mtoto wa kike wazazi wameaswa kuwa karibu na watoto

12 October 2022, 4:08 pm

RUNGWE-MBEYA

NA: SABINA MARTIN

Wazazi na walezi wilayani Rungwe mkoani Mbeya wametakiwa kutenga muda wa kukaa na kuzungumza na watoto wao kuhusu mambo mbali mbali ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili vinavyoendelea katika jamii.

Rai hiyo imetolewa na baaadhi ya watoto wa kike waliohudhuria katika hafla ya maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike kimataifa ambayo kiwilaya yamefanyika katika ukumbi wa John Mwankenja halmashauri ya wilaya ya Rungwe.

Aidha watoto hao wameitaka serikali ya wilaya kupitia ofisi ya ustawi wa jamii kwa kushirikiana na maendeleo ya jamii wakati mwingine kuandaa midahalo itakayowahusisha watoto wa kiume na wanaume kwani wao ndio watekelezaji wakuu wa ukatili wa kijinsia kwa watoto wa kike.

Akisoma risala kwa niaba ya watoto wa kike wilayani hapa mtoto Moza Juma Mahambe amebainisha miongoni mwa changamoto wanazokumbana navyo watoto wa kike kuwa ni pamoja na mimba za utotoni, kufanyishwa kazi ngumu pamoja na tatizo la kukosa haki zao za mirathi katika familia.

Ili kupunguza na kukomesha kabisa vitendo vya ukatili dhidi ya watoto wa kike wilayani hapa Bi. Bupe Sucka Petter ambaye ni askari kutokea dawati la jinsia na watoto Tukuyu ametoa rai kwa watoto wa kike kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili watuhumiwa wanao bainika wachukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria.

Elizabeth Maembe ni afisa ustawi wa jamii wilayani hapa amesema kwamba watoto kukosa chakula shuleni ni moja kati ya sababu zinazopelekea watoto wa kike kuingia katika vishawishi hivyo kupelekea wengi wao kurubuniwa na kujiingiza katika makundi mabaya.

Akizungumza katika hafla hiyo mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Rungwe Dk. Vicent Anney Katibu tawala wa wilaya Bw. Nkondo Bendera amesema kwamba ili kuwafanya watoto wa kike watimize ndoto zao kuna haja ya kuingiza somo la malezi kwa watoto wa shule za msingi hadi elimu ya juu katika mitaala ya elimu.

Kwa Mwaka huu 2022, Kaulimbiu inayoongoza Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike ni; “Haki Zetu ni Hatima Yetu; Wakati ni Sasa”. Kaulimbiu hii inahimiza utoaji wa haki sawa kwa Watoto wote bila ubaguzi katika familia na kwenye jamii.