Chunya yaanza maandalizi mapokezi ya mwenge wa uhuru
16 April 2024, 15:50
Maandalizi yaendelea wilaya ya Chunya kupokea mbio za mwenge wa uhuru utakaopokelewa mwezi wa nane mkoani Mbeya mwaka huu.
Na Hobokela Lwinga
Mkuu wa wilaya ya Chunya Mhe. Mbarak Alhaji Batenga, mapema leo amefungua kikao kazi cha maandalizi ya mbio zaa Mwenge wa Uhuru 2024 Mkoa wa Mbeya, katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Chunya (Sapanjo Hall).
Kikao hicho kimehudhuriwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Chunya Ndugu, Anakleth Michombero, Mratibu wa Mwenge Mkoa Bi Victoria Shao, Maafisa mazingira, Maafisa Mawasiliano serikalini, na Waratibu wa Mwenge kutoka Halmashauri zote za mkoa wa Mbeya.
Katika ufunguzi wake Mhe. Batenga, ameupongeza mkoa wa Mbeya kwa kufanya vizuri katika mapokezi ya mbio za Mwenge za mwaka 2023.
“Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mliyoifanya pamoja kama mkoa katika mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023” alisema Mhe Batenga
Mhe Batenga amewataka waratibu wa Mwenge kufanya tathimini mapema mara tu baada ya matokeo ya mbio za Mwenge wa Uhuru kutoka na sio kusubiria mpaka mwaka mwingine.
Mwenge wa uhuru 2024 katika Mkoa wa Mbeya utapokelewa Agost 24, wilayani Chunya na baadaye kukimbizwa kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya zikitanguliwa na wilaya ya Chunya.