Baraka FM

Miche 1000 kupandwa shule wilayani Rungwe

16 January 2024, 11:07

Na mwandishi wetu

Halmashauri ya wilaya ya Rungwe ikishirikiana na wadau wengine (TFS &Bonde la maji ziwa Nyasa) imeungana na Watanzania wengine katika zoezi la upandaji wa miti.

Zoezi hili limefanyika katika shule mpya ya sekondari Isaka iliyopo katika kata ya Nkunga barabara ya Kiwira-Igogwe.

Ally Said Kiumwa Katibu Tawala Wilaya ya Rungwe ndiye aliyekuwa Mgeni Rasmi katika zoezi hili ambapo amewataka wakazi wa wilaya ya Rungwe kuhakikisha kila kaya inapanda miti ili kutunza uoto wa asili, utunzaji wa mazingira sambamba na kuhakikisha kila mtu anazuia vitendo vyote vya uharibifu wa mazingira ikiwemo kukata miti hovyo na uchomaji moto misitu.

Amesema ili dunia ibaki katika usalama wake kila mtu hana budi kuhakikisha kila wakati anapanda miti ikiwa ni sehemu ya kupata hewa safi, mvua ya kutosha, kuzuia mmomonyoko wa ardhi, na kupandisha kipato cha kaya na taifa kwa ujumla.

Afisa Misitu Halmashauri ya wilaya ya Rungwe Bi.Numwagile Bughali ameeleza kuwa leo jumla ya miche 1000 inatarajiwa kupandwa katika shule hii huku malengo yakiwa ni kupanda jumla ya miche million 1.5 katika mwaka huu wa fedha 2023/24.

Kupitia kitalu chake kilichopo Tukuyu mjini Halmashauri imezalisha miche ya mbao, vivuli, na matunda ambayo hugawa bure kwa mtu mmoja mmoja na taasisi zote kwa ujumla.